HADITHI YA BABA MASUMBUKO SEHEMU YA TANO (5)



                                                                                   HADITHI YA
                                                                                   BABA MASUMBUKO

Mwandishi:PAUL M,YAHILIMA
O788624797
0765084515
Facebook Yahilima PM
                                                                                         SEHEMU YA TANO

Kiongozi mkuu wa sungusungu akiwa amebakiza hatua chache ili atekeleze kilichoamriwa na wananchi,ghafula sauti nzito kutoka kwenye kipaza sauti ilisikika,nilipogeuza macho kutazama sauti ilipotokea yalikuwa ni magari mawili ya kikosi cha polisi cha kuzuia fujo,baada ya ile sauti kuamuru wananchi wajisalimishe kila mmoja alianza kukimbia na kuelekea anapopajua yeye ili kuepusha kukamatwa na polisi,jambo la kwanza nililoliona kuwa ni jema kumwokoa mke wangu mkubwa na mama mkwe ili wasikamatwe na polisi,nilikimbia hadi kwenye mti walipokuwa wamefungiwa nilikimbia kwa haraka nilipofika nikachomoa kisu changu nikakata kamba walizofungiwa

Kimbieni muende nyumbani

Wewe tuache,chanzo cha matatizo yote  haya ni wewe

Kimbieni mtakamatwa

Baada ya kuwapa maelezo yale na nilipoona wanazidi kuwa wabishi niliamua kukimbia kuelekea kwenye msitu uliokuwa karibu na mto,nilikimbia kwa haraka na sikuona askari yoyote aliyekuwa ananifuata na nilipofika kwenye ule msitu niliwakuta wananchi wengi wakiwa wamekimbilia kwenye ule msitu,sauti za mabomu zilikuwa zikiendelea kusikikana kutokana na upepo kuelekea upande ambao tulikuwepo hadi sisi tulijikuta machozi yakitutoka kutokana na mabomu ya machozi yaliyokuwa yakiendelea kusikika,ndani ya ule msitu kila mmoja alikuwa kimya na kila mmoja alionekana akiwa mwenye uoga sana.

Milio ya mabomu ilitulia baada ya muda kama wa saa moja na kwa mbali tukiwa pale msituni tuliziona gari za polisi zikiwa zinapita kwenye barabara ndogo ya vumbi,zikavuka mto na kuondoka kwa mwendo wa kasi sana hadi zikatokomea kwenye upeo wa macho,tuliendelea kukaa pale polini hadi muda wa saa mbili usiku,ngoma ya  kijiji ilipigwa ikiashiria kuwataka wanaume wote wa kijijii kile kukutana,kwa taratibu na kwa umakini mkubwa tulitoka msituni tukiwa na hofu kubwa sana maana hakuna hata mmoja anayependa kuiacha familia yake na kupelekwa gerezani.

Tulifika kwenye uwanja wa mashujaa kwenye mti wa hukumu ambao ni mti mkubwa kuliko yote pale kijijini tukawakuta wananchi wengi wavulana na wazee wakiimba nyimbo za kishujaa kisha mkuu wa sungu sungu akaamuru tuliokuwa tunafika muda ule tupite mbele tukiwa tumepanga msitari ili waweze kukagua nani ambaye amekamatwa  na polisi,kwa hesabu ya haraka jumla tulikuwa watu zaidi ya30 hivi,tukapanga msitari na kila aliyemfikia mkuu wa sungusungu alitaja jina lake kisha anamwagiwa maji ya uvuguvugu anapita aende kusimama kwenye kundi la wananchi,taratibu ule msitari ulizidi kusogea mbele hadi zamu yangu ilifika nikasogea ili nikaguliwe

Naitwa masanja kifula mbute

Haaaaaa! Haaaaa masanja! Masanja!,jamani huyu hapa msaliti aliwafungulia wale wanawake nikiwa namuona kabisa kwa jicho langu

Mimi sikuwafungulia,labda…..

Kabla hata sijamaliza kueleza nilisikia kitu kizito kikitua kichwani mwangu na muda huo huo giza zito likatanda machoni,nilishituka baada ya muda nisioujua nikafungua macho taratibu, kwa mbali nikasikia sauti za watu ila nilipojipapasa nikajikuta nimelowana mwili mzima na fikra zikarudi palepale nikajua kuwa nilikuwa kwenye hatari na hofu ilizidi moyoni mwangu

Leteni maji mmwagie aamke atwambie wako wapi wanawake wake

Sawa mkuu

Niliposikia sauti ile hofu iliongezeka moyoni mwangu maana hakuna mtu aliyekuwa anaogopwa kama yule mkuu wa sungusungu na ukizingatia tayari nimekuwa mtuhumiwa mbele ya wanakijiji wenzangu,maji yaliletwa nikamwagiwa maji mengi hadi sehemu nilipokuwa nimelala kukawa na tope nyingi,niliendelea kujifanya kama bado nimezimia ila nilikuwa nawasikia kila kitu walichokuwa wanaongea,mkuu wa sungusungu aliamuru vijana wake wafuate ng`ombe nyumbani kwangu,walitoka vijana wane wakiwa wanakimbia na baada ya muda mfupi ng`ombe wangu mkubwa kuliko wote aliletwa nilitaka kuamka ili nijitetee lakini nikaamua nikae kimya tu ili niepushe mengi,nikaendelea kujilaza palepale chini huku nawaza juu ya hukumu itakayotolewa juu yangu,ng`ombe aliyeletwa alichinjwa na watu wakachoma nyama kwenye moto uliokuwa umewashwa huku wanakijij wakiendelea kuimba nyimbo za kishujaa.
Baada ya kumaliza kula nyama ya yule ng`ombe,ulikuwa ni usiku wa kama saa saba hivi,kiongozi wa sungusungu alitoa maamuzi kuwa kwa kuwa nimekuwa msaliti na niliwasaidia mke wangu na mama mkwe kwa kuwafungulia kamba walizokuwa wamefungwa,hukumu yangu ilikuwa ni kukatwa mkono wa kulia maana huo mkono ndiyo ulihusika kwenye kukata zile kamba na pia nyumba ya mke wangu mkubwa ilikuwa lazima ichomwe moto ili kumtokomeza kabisa maana yeye ndiye chanzo cha mvua kutokunyesha,baada ya hapo mkuu wa sungusungu aliagiza mtu aje kuniangalia kama nimeamka,Yule mtu alipofika kabla hajanikagua nikazibana pumzi kabisa naye akanikagua kwa kunigeuza geuza

Mkuu,bado hajaamka

Mpumbavu huyo muache,ataanka tu

Baada ya Yule kijana kuondoka nlipata wazo niliamua kutoroka,nikavua shati langu nikasogeza gogo lililokuwa karibu nikalifunika kwa lile shati taratibu nikaanza kujivuta  hadi nyuma ya mti wa hukumu ambao wanakijij hukutana ili kuhukumu wenye makosa,nikaangalia kila upande nikawaza kitu gani nifanye nikafikilia kukimbia kwenda mbali lakini nikaogopa maana wangeniona,nikaamua kupanda juu ya ule mti kabla hata sijafika sehemu ya kujificha vizuri nikamwona mtu anakuja kuangalia nilipokuwa nimelazwa

Haaaaa! Simwoni kaacha gogo tu kalivisha nguo

unasema nini wewe?

Katoroka mkuu.

Niliangalia umati wa watu uliokuwa pale chini ukiwa unakuja  pale nilipokuwa nimelala,wakaanza kutawanyika sehemu mbalimbali ili kunitafuta lakini baada ya dakika 30 ngoma ilipigwa ili kuwarudisha  wananchi waliokuwa wametawanyika kunitafuta hazikupita hata dakika 5 wanakijij wakaanza kurudi kundi kwa makundi muda huo nilikuwa nimejificha kwenye tawi moja la mti kiasi kwamba hakuna hata mmoja mwenye kuweza kuniona

Makamanda hoyeee

Hoyee mkuu

Sasa,twendeni kwake tukachome nyumba yake na tukachukue ng`ombe watano tena,ni sawa au si sawa?

Ni Sawa mkuu!

Baada ya amri ya mkuu wa sungusungu wananchi wote walianza kukimbia kuelekea nyumbani kwangu,nikawaza sana nikaona ni vyema niende nyumbani nikajisalimishe ili wasichome nyumba na kuchukua ng`ombe wangu,nikashuka taratibu kwenye ule mti na kuanza kuwafuata kwa nyuma,kabla sijafika nyumbani nikajibanza kwenye miti ya minyaa huku naangalia kipi wataanza kukifanya,mkuu wa sungusungu akaamuru moto uwashwe na kweli nyumba ya mke wangu mkubwa ambayo ni nyumba ya nyasi ikachomwa moto wananchi wote wakashangilia kwa sauti na wakaanza kuimba nyimbo za ushindi,nikiwa nimejibanza nikashituka baada ya mtu kunigusa mgongoni nikageuka kwa uoga na nilipomwona tu nguvu ziliisha kabisa……………….INAENDELEA
                                                               

Comments

Popular posts from this blog

HADITHI YA BABA MASUMBUKO SEHEMU YA KWANZA (1)

HADITHI YA BABA MASUMBUKO SEHEMU YA NNE(4)

HADITHI YA BABA MASUMBUKO SEHEMU YA TATU(3)